Picha
Siku 1 (18/8/2026)
Siku 2 (19/8/2026)
Siku 3 (20/8/2026)
Siku 4 (21/8/2026)
Ratiba wa kijitabu muhtasari wa mawasilisho
Ratiba
kijitabu chenye muhtasari wa mawasilisho
Matangazo na miito
Mwito wa sita
Jumanne ijayo, hatimaye tutaanza mkutano wa Bantu 11!
Kwa wale watakaohudhuria mjini Ghent, hii hapa ni ramani ya Kampasi ya Ledeganck iliyo karibu na Bustani ya Mimea (Botanical Garden) na Makumbusho ya Chuo Kikuu cha Ghent (GUM), ambapo mkutano utafanyika. Anwani ni Ledeganckstraat 35, 9000 Ghent. Siku ya Jumanne, tunatarajia kuwakaribisha kati ya saa 2:30 na saa 3:20 za asubuhi kwa kahawa ili kukamilisha usajili wenu. Kwa wale waliojiandikisha kwa ajili ya chakula chetu cha jioni na ambao bado hawajalipia, tafadhali leteni kiasi kamili (euro 40) taslimu wakati wa kujisajili siku ya Jumanne asubuhi. Usajili na huduma zote za chakula na vinywaji (kahawa na chakula cha mchana vitatolewa kwa washiriki wote) vitafanyika katika ukumbi wa Palmarium, ambao uko umbali wa mwendo wa dakika chache kutoka kwenye kumbi za mawasilisho (tazama ramani). Tafadhali mpange muda wa kutosha kwa ajili ya matembezi haya mafupi.
Hapa pia mtapata toleo la sasa la ratiba, ambayo nakala yake itajumuishwa kwenye kijitabu cha mkutano. Tafadhali ipitieni upya ili kuhakikisha hukosi mabadiliko yoyote ya dakika za mwisho mwisho. Tumetenga dakika 20 kwa kila wasilisho pamoja na dakika 10 kwa ajili ya maswali na majibu.
Haitawezekana kutumia kompyuta yenu binafsi (laptop) kuwasilisha wakati wa mkutano kutokana na sababu za kiufundi. Tafadhali leteni wasilisho lenu kwenye kifaa cha kuhifadhia data (USB drive) ili liweze kuwekwa kwenye kompyuta ya chuo kikuu kabla ya kipindi chenu kuanza. Pia, haitawezekana kuchapisha nakala za karatasi katika eneo la mkutano. Kuna maduka kadhaa ya uchapishaji jijini Ghent, kwa mfano Print For You na Mister Copy lakini afadhali mje nazo nakala zenu tu. Washiriki waliojiandikisha kuhudhuria mtandaoni watapokea ratiba tofauti yenye viungo vya Zoom. Ikiwa ni mshiriki wa ana kwa ana na ungependa kupokea ratiba hiyo pia, tafadhali utujulishe.
Mnaweza kupakua kijitabu chenye muhtasari wa mawasilisho hapa. Toleo la mwisho litawekwa kwenye tovuti yetu Jumatatu jioni. Ikiwa kuna marekebisho yoyote yanayohitajika, tafadhali mtujulishe haraka iwezekanavyo. Kijitabu hicho cha muhtasari hakitachapishwa.
Kwa usafiri wa umma kwenda Ghent, angalia tovuti ya Shirika la Reli la Ubelgiji (Belgian Railways) hapa kwa ratiba za ndani ya nchi na hapa kwa ratiba za kimataifa. Kwa usafiri wa umma ndani ya Ghent, angalia tovuti ya De Lijn hapa.
Jumanne jioni, tutakaribishwa saa 12:00 jioni (6:00 p.m.) katika ukumbi wa kihistoria wa jiji (Botermarkt 1, 9000 Ghent). Tutatembea mpaka huko katika makundi mawili, tukiondoka saa 11:15 jioni (5:15 p.m.) kamili. Ni mwendo wa takriban nusu saa kwa miguu. Kwa wale wanaopendelea, Elisabeth Kerr ataongoza kundi la tatu litakalotumia basi. Tafadhali tujulishe wakati wa usajili siku ya Jumanne asubuhi kama ungependa kutembea au kutumia basi.
Mwisho, tungependa kutangaza kwamba, kwa ombi la wahariri wa kitabu cha Oxford Guide to the Bantu Languages (OGBL), tutahitimisha mkutano wa Bantu 11 siku ya Ijumaa kwa utambulishaji wa vitabu kuhusu lugha za Kibantu, ikiwemo OGBL yenyewe. Wenzetu waliochapisha kitabu kipya tangu mkutano wa Bantu 10 wanakaribishwa kuleta vitabu hivyo; watapata nafasi ya kuvitambulisha kwa ufupi, kwa njia simulizi, na katika hali isiyo rasmi (dakika 3 kwa kila kitabu) kabla ya kamati ya uongozi kuhitimisha mkutano na kuelekeza mawazo kwenye mkutano wa Bantu 12.
Ikiwa mna swali lolote, tafadhali msisite kuuliza. Ili kurahisisha mawasiliano ya haraka, tutatumia pia kundi letu la WhatsApp la Bantu 11. Ikiwa bado hamjajiunga, mnaweza kujiunga kupitia kiungo hiki: https://chat.whatsapp.com/CMGc2Hso1XNAwNUTsxAS0i.
Tunatarajia kwa hamu kubwa wiki yetu ya pamoja iliyojaa mambo ya lugha za Kibantu.
Mwito wa tano
Bantu 11 itaanza baada ya mwezi mmoja na kidogo. Hapa pana ratiba ya awali ya kwanza. Tumejumuisha tu mawasilisho ambayo tumepokea angalau usajili mmoja uliolipiwa. Ikiwa wasilisho lako halipo ingawa umesajiliwa na kulipa, tafadhali tujulishe haraka iwezekanavyo. Kwa kuwa kuandaa ratiba hii ni kazi ngumu, tunataka kufanya mabadiliko machache iwezekanavyo. Kwa hiyo tutahamisha wasilisho tu ikiwa ni lazima kabisa. Mawasilisho ya mtandaoni yamewekewa alama ya manjano. Tafadhali tujulishe ikiwa tumekosea kwa ku(to)weka alama ya manjano.
Ikiwa bado hujatutumia toleo la Word la mada yako lenye majina na taasisi za waandishi wote, tafadhali lipakie hapa kabla ya mwisho wa mwezi.
Mwisho, tungependa kukukumbusha kuhusu chakula cha jioni cha bufeti cha kozi tatu cha Bantu 11, ambacho tunatoa kwa ushirikiano na Rosi’s Cuisine. Gharama ni €40, itakayolipwa pamoja na ada ya mkutano. Maelezo zaidi kuhusu menyu na jinsi ya kujisajili yanapatikana hapa Mwisho wa kujisajili kwa chakula cha jioni bado ni tarehe 31 Julai 2026.
Mwito wa nne
Bantu 11 inakaribia kwa kasi. Tunatarajia kwa hamu kuwakaribisha nyote mjini Ghent.
Hadi sasa, washiriki zaidi ya 100 wamejisajili rasmi. Hata hivyo, kwa idadi kubwa ya makala zilizokubaliwa, bado hatujapokea muhtasari uliorekebishwa (tarehe ya mwisho ya kuuwasilisha ilikuwa Aprili 1) wala usajili.
Ili kuhakikisha kuwa tukio linaenda vizuri, tunaomba mjisajili kabla ya tarehe 9 Julai, 2026, na kututumia muhtasari wenu uliorekebishwa na mwenye majina kamili ya waandishi. Makala ambazo bado hazina usajili uliolipiwa wala/au muhtasari uliorekebishwa kufikia tarehe hiyo zitaondolewa kwenye ratiba. Hii pia inahusu mawasilisho ya mtandaoni.
Mwisho, tunafurahi kutangaza chakula cha jioni cha bufeti cha kozi tatu cha Bantu 11, ambacho tunatoa kwa ushirikiano na Rosi’s Cuisine. Gharama ni euro 40, itakayolipwa pamoja na ada ya mkutano. Maelezo zaidi kuhusu menyu na jinsi ya kujisajili yanapatikana hapa. Mwisho wa kujisajili ni Julai 31, 2026.
Mwito wa tatu
Jukwaa la usajili mtandaoni kwa ajili ya mkutano wa Bantu11 hatimaye limefunguliwa. Tunasikitika kwa kuchelewa kidogo. Ili kufidia hili, muda wa mwisho wa usajili wa mapema umeongezwa hadi Mei 1, 2026. Tafadhali bofya hapa kukamilisha usajili wako.
Pamoja na ufadhili mdogo wa nje ambao tumeomba, ada za usajili zinalipia gharama mbalimbali, kama vile ukodishaji wa maeneo ya mkutano, vifaa, zana, kahawa na chai wakati wa mapumziko na chakula cha mchana wakati wa siku nne za mkutano, na wasemaji wakuu wanne. Ada zetu za ngazi zinatokana na kanuni ya mshikamano, ambapo washiriki wenye shahada za juu kutoka nchi zenye kipato cha juu husaidia kulipia sehemu ya gharama za washiriki kutoka nchi zenye kipato cha chini na wanafunzi (wa udaktari). Washiriki katika ngazi ya juu zaidi pia huchangia kugharamia idadi teule ya washiriki bora kutoka nchi zenye kipato cha chini, ambao ada zao za ushiriki hugharamiwa kikamilifu na kamati ya maandalizi. Orodha ya nchi za kipato cha chini zinazostahili inapatikana hapa.
Kwa sasa, tunajivunia kutangaza wazungumzaji wetu wakuu wanne: Thera Marie Crane, Rozenn Guérois, Amani Lusekelo, na Cesar Fortes-Lima. Majina ya mawasilisho yao makuu pamoja na orodha ya mawasilisho yaliyokubaliwa yote vinapatikana hapa.
Pia tungetaka kuwakumbusha waandishi wote kutuma toleo lisilo la siri la muhtasari wao kufikia tarehe 1 Aprili (kufuatia maelekezo yaliyomo kwenye barua pepe ya kukubaliwa).
Maelezo zaidi kuhusu masharti ya viza na taarifa nyingine muhimu kwa watafiti wasafirio kwenda Ubelgiji yanapatikana hapa.
Hatimaye, tuna furaha kukujulisha kuwa tumefikia makubaliano na mashirika ya ndege ya Kundi la Lufthansa (Lufthansa, SWISS, Austrian, Brussels Airlines, Eurowings, Edelweiss, Discover) ili kuboresha gharama zako za usafiri. Mtandao wao mpana wa njia unao na takriban maeneo 310 duniani kote na unaojumuisha safari za kuvuka Atlantiki zinazofanywa na Air Canada na United unapatikana kwako. Bofya hapa kuonyesha viwango vilivyopunguzwa. Vinafaa kwa safari za ndege hadi wiki moja kabla na wiki moja baada ya tukio.
Mwito wa pili
Wito wa ikisiri za mawasilisho kwa Mkutano wa 11 wa Kimataifa wa Lugha za Kibantu (Bantu 11) katika Chuo Kikuu cha Ghent (Agosti 18-21, 2026) sasa umefunguliwa. Mkutano huo utajumuisha kikao kikuu kinachokaribisha mawasilisho kuhusu kipengele chochote cha lugha za Kibantu, pamoja na warsha kumi na moja zinazohusika mada maalum (tazama maelezo ya warsha hapa).
Tarehe ya mwisho kwa ikisiri ya mawasilisho ni Desemba 8, 2025 (23:59 UTC/GMT+1). Kila mtu anapaswa kutoa ikisiri zisizoongeza mbili na moja kati yake tu iwe ya mtu peke yake. Ikisiri iwe na ukurasa 1 wa maandishi (ikiwemo takwimu/jedwali/mifano ya lugha) na ukurasa 1 wa ziada kwa marejeleo, katika fonti ya Charis SIL ya pt 11 au fonti ya Times New Roman ya pt 12, yenye nafasi moja, yenye pembezoni mwa kawaida za A4 (cm 2.54). Mawasilisho yanaweza kutolewa ana kwa ana au mtandaoni. Kutakuwa na ada ya mkutano iliyopunguzwa kwa wanafunzi (ikiwemo wanafunzi wa PhD) na washiriki kutoka nchi zenye kipato cha chini.
Lazima ikisiri ipelekwe kupitia jukwaa la EasyAbs tu. Kama bado huna akaunti ya EasyAbs, utengeneze kwanza akaunti ya bure kwenye EasyAbs, kisha upeleke ikisiri yako kwenye mkutano wa Bantu 11, ukifuata miongozo ya uumbizaji hapo juu. Tafadhali hakikisha kwamba faili ya muhtasari (ikiwa ni pamoja na jina la faili) isiwe na jina na iwe katika muundo wa .pdf. Tafadhali ongeza alama ya warsha husika (k.m. ‘WS01’) au tumia ‘GS’ kwa wasilisho la kikao kikuu, na ongeza maneno muhimu 3-5 yanayoelezea wasilisho lako (k.m. ‘fonolojia’, ‘sociolinguistics’, ‘Southern Bantu’). Ikiwa unalipeleka wasilisho lililoandikwa na mtu mmoja, tafadhali onyesha ikiwa unatarajia kuwepo Ghent. Ikiwa unalipeleka wasilisho lililoandikwa na zaidi ya mtu mmoja, tafadhali onyesha ni waandishi wangapi wanatarajia kuwepo Ghent.
Ikiwa una matatizo yoyote na jukwaa la EasyAbs, jaribu kuonyesha upya ukurasa, tumia programu tofauti ya mtandaoni, angalia tovuti ya EasyAbs (https://easyabs.linguistlist.org/about/), au wasiliana na kamati ya maandalizi ya Bantu11 kwa Bantu11@UGent.be.
Taarifa zaidi zinaweza kupatikana kwenye tovuti ya mkutano. Maswali yote yanaweza kutumwa kwa Bantu11@UGent.be.
Tunatarajia kupokea ikisiri zenu na kuwakaribisha nyote Ghent!
Mwito wa kwanza
Tovuti ya Kongamano la Bantu11 iko mtandaoni sasa. Hapa utapata habari muhimu zote ambazo zitasasishwa mara kwa mara. Kwa sasa, inakufahamisha kuhusu mahali pa Kongamano na tarehe muhimu za kukumbuka.
Tarehe ya mwisho ya kwanza ni 15 Oktoba 2025 (23:59 UTC/GMT+2), kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya warsha. Tutumie kwa Bantu11@UGent.be kufikia wakati huo ikisiri yako yenye maneno yasiyozidi 1000 yakiwemo marejeleo na mstari wa kwanza wa sentensi za mifano ya lugha. Tafadhali taja majina ya wasimamizi wa warsha, lakini USIJUMUISHE orodha ya mawasilisho/wawasilishaji. Tutachapisha warsha zilizochaguliwa kwenye tovuti ya Kongamano kabla ya tarehe 1 Novemba 2025.
Tarehe ya mwisho ya pili kwa ikisiri ya mawasilisho, ni tarehe 1 Desemba 2025 (23:59 UTC/GMT+2). Utoaji wa ikisiri utafunguliwa kuanzia tarehe 1 Novemba hadi tarehe hii ya mwisho. Tafadhali usitutumie mapendekezo yoyote ya wasilisho kabla ya kipindi hiki, ili uweze kutujulisha kama unataka kushiriki katika warsha au katika kikao cha jumla. Maelezo zaidi kuhusu utaratibu wa utoaji wa ikisiri utafuata baadaye.
Mahali pa mkutano patakuwa Chuo cha Ledeganck karibu na Makumbusho ya Chuo Kikuu cha Ghent na Bustani ya Mimea. Chuo hiki kiko karibu na kituo cha Gent-Sint-Pieters, kituo kikuu cha treni cha jiji, ambacho kimeunganishwa moja kwa moja na Uwanja wa Ndege wa Brussels na kinachoweza kufikiwa kutoka kwa vituo vikuu vyote vya treni vya Ulaya, ikiwemo kituo cha Leiden (Uholanzi), ambapo Kongamano la 55 la Lugha na Isimu za Kiafrika (CALL 2026) litafanyika kuanzia tarehe 24 Agosti hadi 2026 Agosti. Jiji pia lina kituo cha Flixbus karibu na kituo cha gari moshi cha Gent Dampoort, ambacho kimeunganishwa vyema na miji mikubwa ya Ulaya, ikiwemo Rotterdam na The Hague, ambapo kuna matreni yaelekeayo Leiden.
Tafadhali bofya hapa kwa kuona mahali pa kukaa palipo karibu Chuo cha Ledeganck. Kwa mahali pa kukaa pengine na mambo ya kufanya, tafadhali tembelea tovuti ya Tembelea Gent.
Tunatazamia kupokea mapendekezo yenu ya warsha na kuwakaribisha nyote Ghent!
Tangazo la kwanza
Timu ya BantUGent ina furaha kukukaribisheni jiji la Ghent (Ubelgiji) kwa Kongamano la 11 la Kimataifa la Lugha za Kibantu (Bantu11). Litafanyika kuanzia Agosti 18 hadi Agosti 21, 2026, kabla tu ya Kongamano la 55 la Lugha na Isimu za Kiafrika (CALL 2026) huko Leiden (Uholanzi) kuanzia Agosti 24 hadi Agosti 26, 2026. Mwito wa kwanza wa mawasilisho na warsha utatangazwa mwezi mwa Septemba 2025. Mkiwa na maswali tafadhali yatume kwa anwani ifuatayo: Bantu11@UGent.be.
Mahali
Mkutano wa Bantu 11 utafanyika Chuo cha Ledeganck karibu na Makumbusho ya Chuo Kikuu cha Ghent na Bustani ya Mimea. Chuo hiki kiko karibu na kituo cha Gent-Sint-Pieters. Madokezo ya mahali pa kukaa karibu na Chuo cha Ledeganck yanapatikana hapa. Mahali pengine pa kukaa na mambo ya kufanya jijini yanapatikana kwenye tovuti ya Tembelea Gent.
Tarehe muhimu
- Oktoba 15, 2025: tarehe ya mwisho ya warsha
- Novemba 1, 2025: tarehe ya tangazo la warsha zilizochaguliwa
- Desemba 1, 2025: tarehe ya mwisho ya mawasilisho
- Januari 15, 2026: arifa za kukubalika
- Machi 18, 2026: ufunguzi wa usajili (wa mapema hadi Mei 1)
- Julai 9, 2026: tarehe ya mwisho ya usajili chuoni
- Agosti 17, 2026: tarehe ya mwisho ya usajili mtandaoni
- Agosti 18-21, 2026: mkutano
Warsha
Mkutano wetu utajumuisha kikao cha jumla ambacho kitakaribisha mawasilisho kuhusu kipengele chochote cha lugha za Kibantu, pamoja na warsha zifuatazo:
- WS01 Unravelling the knots of not: Exploring lesser-known negative patterns in Bantu
- WS02 Swahili, Sabaki, and Beyond:Integrating New Data and Perspectives on the East African Coast
- WS03 Clause Chaining in Bantu languages: Narrative verb sequences with and without-morphological marking
- WS04 Renewing Bantu Lexical Reconstruction
- WS05 Interdisciplinary perspectives on Bantu language history
- WS06 The effects of maximality constraints on verb structure
- WS07 Ethnolinguistics, Ethnobiology and Biodiversity / WS07 Ethnolinguistique, ethnobiologie et biodiversité
- WS08 Phonetic and phonological documentation: the role of Bantu in establishing new standards for the discipline
- WS09 Irregular sound change in Bantu
- WS10 Advances and developments in cross-Bantu typology: Empirical, comparative and methodological approaches
- WS11 Nominal Classification in Bantu or the Semantax of the Noun / WS11 Classification nominale en bantou ou la semantaxe du nom
Mawasiliano
Ututumie barua pepe kwa njia ya Bantu11@UGent.be. Ili kujiunga na kikundi cha WhatsApp cha Bantu 11, bofya hapa.
Kamati ya maandalizi
- Paulin Baraka Bose (UGent)
- Arnaud Bizongwako (UGent-UBurundi)
- Koen Bostoen (UGent)
- Pieter De Coene (UGent)
- Maud Devos (Royal Museum for Central Africa)
- Sebastian Dom (UGent)
- Heidi Goes (UGent)
- Hilde Gunnink (UGent-ULeiden)
- Elisabeth Kerr (UGent)
- Margot Luyckfasseel (UAntwerpen)
- Lorenzo Maselli (UGent-UMons)
- Edward Ntonda (UGent-UNanterre-LLACAN)
- Sara Pacchiarotti (UGent)
- Chrisnah Renaudot Mfouhou (UGent)
- Nina van der Vlugt (UGent)
- Aron Zahran (UGent-INALCO-LLACAN)
Kamati ya kisayansi
- Koen Bostoen (UGent)
- Maud Devos (Royal Museum for Central Africa)
- Gratien Atindogbe (University of Buea)
- Lotta Aunio (University of Helsinki)
- Hannah Gibson (University of Essex)
- Claire Halpert (University of Minnesota)
- Amani Lusekelo (University of Dar es Salaam College of Education)
Wafadhili
- Margot Luyckfasseel (UAntwerpen)
- Lutz Marten (School of Oriental and African Studies London)
- Mantoa Motinyane (University of Western Cape)
- Atikonda Mtenje-Mkochi (Malawi University of Science and Technology)
- Mark Van de Velde (LLACAN)
- Nobuko Yoneda (Osaka University)
- Alexander Zheltov ( Saint Petersburg State University)
